Wenyeviti wa vijiji na vitongoji wa wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya Serikali.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, wakati akifungua mafunzo maalumu kwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji yaliyofanyika wilayani hapa.
Mafunzo hayo ya siku mbili yamelenga kuwaongezea viongozi hao uelewa na uwezo, kujua majukumu yao ya msingi katika utendaji kama wenyeviti wa vijiji na vitongoji ili kuongeza kwa ufanisi katika kazi zao.
Mhe.Kasilda pia amewataka viongozi hao kusimamia kwa uwazi mapato na matumizi ya vijiji vyao, kusimamia utekelezaji wa miradi inayotekelezwa.
"Simamieni kuhakikisha kuwa Miradi yote inaendeshwa kwa uwazi, mapato na matumizi yasomwe kwa wananchi. Alisema Mhe. Kasilda.
Mkufunzi wa mafunzo hayo, Dkt. Muhsin Danga, Mhadhiri kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, amesema mafunzo hayo yanajikita katika mada za uongozi na utawala bora, muundo na sheria za uendeshaji wa Serikali za Mitaa, usimamizi wa fedha na ardhi, pamoja na uibuaji na upangaji wa mipango endelevu.
Baadhi ya wenyeviti wameshukuru kwa mafunzo hayo na kuahidi kwenda kufanya kazi kulingana na maelekezo ya mafunzo hayo.
Mafunzo haya yaliyoandaliwa na Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI yamewahusisha wenyeviti 100 wa vijiji na wenyeviti 503 wa vitongoji vya Wilaya ya Same.
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.