Bodi ya Pamba nchini (TCB)) imetoa zawadi ya majiko ya gesi kwa wakulima hodari wa Pamba Wilayani Same ambao wameweza kuzingatia kanuni za kilimo bora cha Pamba kilichowezesha uzalishaji wa zaidi ya kilo 1,500 kwenye ekari moja.
Bodi hiyo pia imetoa zawadi ya vitenge na kanga kwa maafisa Ugani Wilayani Same kama sehemu ya kutambua mchango wao katika kuongeza uzalishaji wa zao la Pamba.
Wakulima walionufaika na zawadi hizo ni Gabriel Mbwambo na Praise Mbwambo ambao wote wanatoka Kata ya Kisiwani na maafisa ugani waliopatiea zawadi ni Debora Mtati na Fatuma Sadala.
Akikabidhi zawadi hizo Afisa Kilimo kutoka Bodi ya Pamba Bw. Alphonce Ngawagala
alisema utoaji wa zawadi ni motisha kwa Wakulima na maafisa ugani ili kuchochea ongezeko la uzalishaji wa Pamba hapa nchini.
"Bodi ya Pamba itaendelea kutoa zawadi kama motisha kwa wakulima wa pamba ili zao hili liweze kuzalishwa kwa wingi katika maeneo mengi wilayani Same na nchini kwa jumla"alisema Bw.Ngawagala na kuongeza kuwa mwaka jana Bodi hiyo ilikabidhi zawadi ya Trekta yenye thamani ya mil 55 kwa mkulima Gabriel Mbwambo baada ya kuibuka mkulima bora wa Pamba kwenye Kanda hii.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Bw.Wambura Yamo aliwapongeza Wakulima waliofanya vizuri msimu huu na kuwataka kuongeza jitihada ili zao la Pamba lienee maeneo mengi Wilayani Same."Uzalishaji wa Pamba unapoongezeka hata mapato ya serikali yanaongezeka kupitia ushuru wa mazao na Serikali inapoongeza mapato inaboresha utoaji wa huduma za kijamii.
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.