Wafugaji Wilayani Same wametakiwa kutoa ushirikiano kwa maafisa mifugo wakati huu ambao kunafanyika zoezi la utoaji wa chanjo za mifugo zenye ruzuku ya Serikali ili kukinga mifugo na kuku dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Afisa Mifugo na kilimo Wilayani Same Bw.Ninzari Idd amesema zoezi hilo la chanjo ya Ruzuku linakwenda sambamba na zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kuvishwa hereni maalumu za kielektroniki ili iweze kutambuliwa popote itakapokuwepo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan katika juhudi za kuboresha uzalishaji wa mifugo hapa nchini alizindua kampeni ya Kkitaifa ya utoaji chanjo za mifugo zenye ruzuku ya Serikali tarehe 16 Juni 2025 Wilayani Bariadi (Simiyu).
Chanjo hizi ni dhidi ya Homa ya Mapafu ya Ng’ombe (CBPP) ambayo inatolewa kwa Tsh 500 kwa ng’ombe mmoja badala ya Tsh 1000 na kwa upande wa mbuzi, chanjo ya Sotoka ya mbuzi itatolewa kwa Tsh 300 kwa mbuzi mmoja badala ya Tsh 500 ya bei ya soko. Aidha chanjo ya kuku aina ya Tatu moja ambayo ni dhidi ya magojwa ya Ndui, Mafua na kideri yanayoathiri kuku inatolewa bure (bila malipo).
Bw.Ninzari amesema faida za kampeni hii ya kitaifa ya utoaji chanjo na utambuzi wa mifugo ni pamoja na kuboresha afya za mifugo na uzalishaji, kuwa na uhakika wa masoko ya mifugo ndani nan je ya nchi na kuzuia wizi wa mifugo.
Zoezi la utoaji wa chanjo za mifugo Wilayani Same lilianza Julai 4, 2025 kwa utoaji wa chanjo aina ya Tatu moja kwa kuku dhidi ya magonjwa ya Ndui, Mafua makali na kideri/mdondo ambapo hadi mwanzoni mwa mwezi Oktoba 2025, jumla ya kuku 202,401 wamechanjwa na lengo ni kufikia kuku 220,000.
Ambapo kwa upande wa Ng,ombe jumla ya Ng’ombe 24,364 wameshachanjwa na kuwekwa hereni za kielekroniki kati ya ng’ombe 130,000 wanaotarajiwa kuchanjwa katika Wilaya ya Same.
Mfugaji John Samweli Mamasita wa Kata ya Ruvu amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea chanjo wa mifugo yenye ruzuku kwani imewapunguzia gharama hivyo itawezesha mifugo yote kuchanjwa.
Naye Mfugaji Yohana Kiroya ambaye anasema tayari mifugo yake imeshapatiwa chanjo na anaendelea na zoezi la uwekaji hereni za kielektronik ameishukuru Serikali kwa kuwapatia ruzuku ya Chanjo.
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.