Nawatakia heri ya Mwaka Mpya 2026 Wananchi wote wa Wilaya ya Same. Mwaka 2025 umemalizika salama na ninashukuru kwa ushirikiano mkubwa mlioutoa kwa Serikali katika kuhakikisha kuwa masuala mbalimbali ya maendeleo yanasonga mbele.
Msimu wa sherehe mbalimbali za mwisho wa mwaka tumeumaliza, napenda kuchukua nafasi hii kuwakaribisha tena kwenye ujenzi wa Taifa letu la Tanzania. Napenda kuwakumbusha ndugu zangu wa Wilaya ya Same kwamba jukumu kubwa liliopo mbele yetu kwa sasa ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wanaripoti shuleni bila kukosa.
Kwenye Wilaya yetu ya Same Jumla ya wanafunzi 4,305 wamechaguliwa kujiunga na elimu ya Sekondari mwaka 2,026, kwahiyo wanafunzi wote waliochaguliwa tunataka kuwaona shuleni.
Kwa kutambua kuwa elimu ni msingi bora wa maisha ya mtoto tayari wilaya inayo shule na madarasa ya kutosha kupokea wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na Sekondari. Tukumbuke kuwa Serikali inatekeleza Sera ya Elimu bure ili kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata fursa ya kupata elimu bila kuwa na kisingizio chochote, hivyo hakuna sababu ya mzazi kutompeleka mtoto shule.
Niwakumbushe pia wazazi wenye watoto wenye umri wa kuanzia miaka mitano kuhakikisha kuwa wanawaandikisha darasa la awali na darasa la kwanza, uandikishaji umeanza mwezi Desemba 2025 na utakamilika Machi 31, 2026.
Serikali imetoa muda wa kutosha kwa wazazi kuhakikisha kuwa wanawaandikisha kuanza darasa la kwanza watoto wote wenye umri wa kwenda shule, wazazi mtambue kuwa ni kosa kutompeleka mtoto shule.
Kila mtoto ana haki ya kupata elimu hivyo kila mzazi atimize wajibu wake wa kuhakikisha kuwa anampeleka mtoto shule na pia kuhakikisha anafuatilia maendeleo ya mtoto wake shuleni.
Mwaka huu tunatarajia kuandikisha wanafunzi 5,256 darasa la awali na wanafunzi 5,542 darasa la kwanza na hadi kufikia Januari 23, 2026 kwa darasa la kwanza tumefikia asilimia 96 ya uandikishaji na darasa la awali tumefikia asilimia 105.
Elimu ni ufunguo wa maisha, Mzazi hakikisha unampatia mwanao ufunguo.
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.