Vijana waliofuzu toka Wilayani Same kwenda ngazi ya Mkoa (Kilimanjaro ) kushiriki mashindano ya Michezo kwa Shule za Sekondari hapa nchini (UMISSETA) wametakiwa kujituma kwenye mashindano hayo ili waweze kuleta vikombe vya ushindi Wilayani Same na pia kuteuliwa kuunda Timu ya Mkoa itakayoshiriki mashindano ya Taifa.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Same Bi.Upendo Wella wakati akifunga kambi ya Wilaya ambapo wanafunzi 120 wamefuzi kushiriki ngazi ya Mkoa.
Amewataka wachezaji hao kujituma kikamilifu wawapo kambini ili waweze kushinda wengi na kuunda Timu ya Mkoa ambayo itashiriki mashindano ngazi ya Taifa Mkoani Iringa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Bw.Jimson Mhagama amewataka vijana hao kuwa na nidhamu wakati wote wawapo kambini.
Afisa Michezo Wilaya ya Same Bw.Nevile Nyange amesema wachezaji waliofuzu wanawakilisha Mpira wa Miguu,Mpira wa Wavu na Mpira wa Mikono.
Katika hafla hiyo Meneja wa NMB Tawi la Same Bw.Saad Masawila alikabidhi jezi ya Mpira wa Miguu seti moja kwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Same Bi.Wella kwaajili ya vijana wanaoshiriki mashindano ya UMISSETA.
NMB imeahidi pia kuwafungulia akaunti na kuwawekea fedha za kianzio pamoja na kuwanunulia sare ya shule moja wanafunzi wote watakaofuzu kushiriki mashindano hayo ngazi ya Taifa.
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.