Mkuu wa Wilaya ya Same Mheshimiwa Kasilda Mgeni amezindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria bure kwa wananchi utakaotolewa kupitia Mama Samia Legal Aid Campaign ambao utawasaidia wananchi wenye changamoto zinazohitaji msaada wa kisheria ikiwemo kupatiwa msaada wa mawakili kuwasimamia Mahakamani.
Akizindua Kampeni hiyo Mhe. Kasilda ametoa Wito kwa Wananchi wa Same wenye changamoto za Kisheria kutumia fursa hiyo ili waweze kusaidiwa.
"Wale wote wenye changamoto za kisheria na wale wasio na uwezo wa kuajiri mawakili wa kuwawakilisha mahakamani au kuwaandalia nyaraka za kisheria waje kuwasilisha changamoto zao mbele ya timu ya msaada wa kisheria"alisema
Amesema kampeni hiyo inatarajiwa kupunguza malalamiko ya kisheria kwa wananchi pamoja na kutoa elimu kwa umma.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Wakili Upendo Kivuyo, amesema huduma zitakazotolewa katika kampeni hiyo ni pamoja na kusuluhisha migogoro ya ndoa na talaka, migogoro ya ardhi, mirathi, unyanyasaji wa kijinsia, haki za binadamu, pamoja na masuala ya utawala bora.
Aidha, ameeleza kuwa huduma hizo zitatolewa kwa njia ya ushauri, usuluhishi na hata uwakilishi mahakamani pale inapohitajika, ili kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake kwa wakati.
Kampeni ya msaada wa kisheria bure kwa wananchi (Mama Samia Legal Aid Campaign) iliasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mwaka 2023 kwa lengo la kutoa msaada kwa kisheria kwa wananchi wasio na uwezo wa kuajiri mawakili ambayo inatekelezwa kwa miaka mitatu hadi kufikia mwezi Februari 2026 katika maeneo yote nchini.
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.