Wananchi Wilaya ya Same wametakiwa kuzingatia ulaji wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi ambavyo vinasaidia kuboresha afya zao.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Same Bi.Upendo Wella wakati akizungumza na wadau mbalimbali waliohudhuria kikao cha elimu ya matumizi ya vyakula vilivyoongezwa virutubishi.
Bi. Upendo alisema elimu ya lishe inayotolewa kwa wadau ina lengo la kuhakikisha kwamba Taifa linakuwa na watu wenye afya njema hususan kina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.
“Kikao hiki ni mahususi kwa ajili ya kupata kwa kina elimu ya lishe na matumizi ya vyakula vilivyoongezwa virutubishi kama unga wa sembe, dona, ngano na maharage lishe” alisema
Afisa Lishe Mkoa wa Kilimanjaro Bi.Rehema Napengwa,alisema hali ya udumavu kwa watoto kwenye Mkoa wa Kilimanjaro ni asilimia 20 na hali ya udumavu kitaifa ni asilimia 30.
Alisema ili kuepuka udumavu ni vizuri kuzingatia aina ya vyakula vinavyotumiwa na mjamzito na mtoto kwa muda wa siku 1,000 tangu siku ya kwanza ya ujauzito kwani udumavu hutokea iwapo lishe ya mtoto haitazingatiwa kwa muda huo.
"Udumavu kwa watoto unatokea kwenye kipindi cha siku 1,000 tangu mimba kutungwa ambapo kipindi hicho ni kipindi ambacho mzazi anapaswa kuzingatia sana lishe” amesema Bi.Rehema
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Mheshimiwa Yusto Mapande, amesema wananchi wanapaswa kujifunza kwamba zile siku 1,000 za awali za mimba kutungwa mpaka anazaliwa mtoto ni siku muhimu za kuokoa maisha yake kiafya na kiakili hata atakapokua mtu mzima.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Bw. Jimson Mhagama aliwataka wafanyabiashara wa unga kuhakikisha kuwa wanaongeza virutubishi kwenye unga wanaouzalisha.
Kikao hicho kilibebwa na kaulimbiu isemayo”Lishe sio kujaza tumbo…zingatia unachokula”.
The Way Through Mkomazi Nationa Park or District Hospital(Kibacha Rd)
Sanduku La Posta: P.O.Box 138
Simu ya mezani: +255 27 2758034
Simu Ya Mkononi: +255 717657681
Email: ded@samedc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.