Mkuu wa Wilaya ya Same, Mheshimiwa Kasilda Mgeni, amewataka wafanyabiashara kuendelea kutumia mashine za kielektroniki za kodi (EFD) ili kuhakikisha kila mteja anapata risiti ya mashine anapokuwa amefanya manunuzi yoyote.
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Ushauri wa Kodi cha Wilaya, Mheshimiwa Kasilda alisisitiza kuwa ni jukumu la kila mfanyabiashara kutoa risiti kwa kila mauzo anayofanya, huku akiwaasa wateja kudai risiti wanaponunua bidhaa.
“Tunatakiwa kuendelea kuwaelimisha wafanyabiashara kutumia mashine za EFD, kutoa risiti kwa wateja huku wateja wakisisitizwa kudai risiti wanaponunua bidhaa, ili kulinda mapato ya serikali yasipotee,” alisema Mhe. Kasilda.
Akizungumza kwenye kikao hicho Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Same, Eliapenda Mwanri, alieleza kuwa Taasisi hiyo imefanikiwa kuvuka lengo la makusanyo la Shilingi bilioni 8.04 kwa kipindi cha Julai 2024 hadi Mei 2025, ambapo walifanikiwa kukusanya bilioni 8.1.
Bw. Mwanri aliongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na utoaji wa elimu kwa walipakodi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari na msisitizo wa matumizi ya mashine za EFD.
Kikao cha kisheria hufanyika mara mbili kwa mwaka ikiwa na lengo la kuangalia mwenendo wa makusanyo ya mapato katika Wiilaya na kuweka mikakati ya kuongeza ukusanyaji wa mapato ambapo huwakutanisha wafanyabiashara,viongozi na Mamlaka zinazokusanya mapato ya Serikali.
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.