Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mheshimiwa Nurdin Babu amewataka wananchi wa Mkoa huo kutunza vyanzo vya maji pamoja na mazingira yanayowazunguka kwa kuotesha miti kwa wingi na kuepuka kufanya shughuli za kilimo karibu na vyanzo vya maji.
Mkuu wa Mkoa ametoa maelekezo hayo kwenye ziara yake ya siku mbili aliyoifanya katika Wilaya ya Same ambapo amesema uharibifu wa mazingira unaathiri tabia nchi ambapo husababisha madhara makubwa kwa viumbe hai wakiwemo binadamu.
Amesema uharibifu wa mazingira unasababisha njaa maana misimu ya kilimo inavurugika na pia huleta ukame na hivyo kusababisha mifugo kufa kwa kukosa malisho.
"Otesheni miti pembezoni mwa barabara zote,otesheni miti mingi kuzunguka vyanzo vyote vya maji ili kuhakikisha kwamba kijani ya Kilimanjaro inarudi" alisema Mheshimiwa Babu.
Amesema lengo lake ni kuhakikisha kuwa Hali ya Kijani iliyokuwa imezoeleka inarudi katika Mkoa wa Kilimanjaro.
"Ni kweli kwamba mti ni wako na umeuotesha wewe na umeutunza wewe lakini huruhusiwi kuukata bila kuwa na kibali cha Serikali "alisema Babu.
Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Same Mheshimiwa Kasilda Mgeni alimuahidi Mkuu wa Mkoa kufuatilia agizo hilo na kuhakikisha kuwa miti inaendelea kupandwa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo.
"Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tumepokea maelekezo yako na tunaahidi kuendelea na jitihada za kupanda miti katika maeneo yote"alisema Mkuu wa Wilaya
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa alitembelea Shule ya Msingi Dimbwi ambapo akikagua madarasa matatu ya Mradi wa Boost,Ujenzi wa Daraja linalounganisha Kata za Bwambo na Mpinji pamoja na Uzinduzi wa Jengo la mama na mtoto la Kituo cha Afya Bwambo.
Miradi mingine aliyoitembelea ni pamoja na Ukaguzi wa ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi ya Kisima,Ujenzi wa Hospitali Mpya ya Wilaya na Mradi wa Maji Mabilioni na Kijomu.
The Way Through Mkomazi Nationa Park or District Hospital(Kibacha Rd)
Sanduku La Posta: P.O.Box 138
Simu ya mezani: +255 27 2758034
Simu Ya Mkononi: +255 717657681
Email: ded@samedc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.