Wananchi wa Jimbo la Same Mashariki sasa wanatarajia kupata huduma ya uhakika ya umeme kufuatia kukarabatiwa kwa kituo cha kupokea, kupooza na kusambaza umeme kilichopo katika Kata ya Maore.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Same, Mhandisi Fabian Ruhumbika wakati Mkuu wa Wilaya ya Same Mheshimiwa Kasilda Mgeni alipofanya ziara kukagua ukarabati wa Kituo hicho ambao unagharimu shilingi bilioni 3.3.
Mhandisi Ruhumbika amesema kukamilika kwa mradi huo kutachochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi kutokana na kuongezeka kwa uwezo wa umeme kutoka megawati 2 hadi megawati 10.
Mhe. Kasilda amepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutekeleza Mradi huo ambao ameutaja kama mkombozi wa uchumi wa wananchi.
Serikali imedhamiria ifikapo mwishoni mwa mwaka huu Vijiji vyote hapa nchini viwe vinafikiwa na umeme.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 hadi kufikia Septemba 2024 Jumla ya Vijiji 12,240 Kati ya 12,318 tayari vimeshafikiwa na Umeme ambavyo ni sawa na asilimia 99.37.
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.