Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu, amekemea tabia ya baadhi ya wafugaji kulisha mifugo yao kwenye miti inayopandwa katika maeneo mbalimbali Mkoani humo ambapo ameagiza mamlaka za Serikali kutaifisha mifugo Yote itakayokamatwa ikila miti iliyooteshwa.
Mhe. Babu ametoa onyo hilo Machi 19, 2024 Wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro wakati akifungua warsha kuhusu masuala ya uhifadhi wa rasilimali za misitu ikiwa ni sehemu ya matukio kuelekea kwenye maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji Miti Kitaifa inayofanyika Machi 21 wilayani Same, Kilimanjaro.
"Sisi tunaotesha miti lakini wenzetu.wanakuja kulisha mifugo,naagiza Wilaya zote za mkoa wa Kilimanjaro kutaifisha mifugo yote itakayokutwa inakula miti iliyooteshwa"aliagiza Mhe.Babu
Amesema misitu imekuwa na manufaa mengi na kuwa fursa zake zimekuwa zikiongezeka ikiwamo teknolojia ya hewa ukaa na kuwa wananchi wakizitambua fursa hizo watahamasika katika utunzaji wa misitu kwa ajili ya fursa za kiuchumi.
“Misitu inachangia asilimia 3 ya pato la Taifa, inatupatia vifaa vya ujenzi,inasaidia upatikanaji wa mvua,miti inazuia mmomoyoko wa udongo na pia Misitu ni makazi ya wanyama hivyo hatuna budi ya kuhakikisha misitu inahifadhiwa.”alisema
Mkuu wa Mkoa alishauri Elimu kuhusu muhimu wa Misitu itolewe kwa wadau mara kwa mara ili kuwezesha utunzaji wa misitu na upandaji Wa miti Kwa wingi.
Babu amesema Wilaya ya Same ni miongoni mwa wilaya zilizoathirika na ukataji holela wa miti na kilimo kisichofuata taratibu ya mazingira.
Katika kuirejesha Wilaya ya Same na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla kuwa ya kijani, Mhe. Babu alimuagiza Katibu Tawala Mkoa huo kusimamia kwa ukaribu kampeni za upandaji miti ili ipandwe ya kutosha.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni alisema Wilaya ya Same imekuwa ikimuunga mkono Rais Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa kuhakikisha wanahifadhi mazingira kwa kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
"Wilaya yetu imezindua kampeni ya upandaji miti ili kuifanya Same ya Kijani na tayari tumepanda miti kandokando ya barabara kuanzia mwanzo hadi mwisho wa wilaya na mpaka sasa zaidi ya miti laki tano imeshapandwa"alisema Mkuu wa Wilaya.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ufugaji Nyuki, Bw. Daniel Pancras amesema Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inajukumu kubwa la kuhamasisha upandaji miti pamoja na kuelimisha juu ya upandaji miti ili watanzania wajue namna bora ya kupanda na kutunza miti
The Way Through Mkomazi Nationa Park or District Hospital(Kibacha Rd)
Sanduku La Posta: P.O.Box 138
Simu ya mezani: +255 27 2758034
Simu Ya Mkononi: +255 717657681
Email: ded@samedc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.