Katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya bila kikwazo cha kifedha, Wilaya ya Same imezindua rasmi zoezi la uandikishaji wa Bima ya Afya kwa Wote. Uzinduzi huo ulifanyika Kata ya Stesheni, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Afya ya kuwafikia wananchi wote kwa huduma za afya.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Same, Bi. Mamndolwa Gembe, amewataka watumishi wa afya katika maeneo lengwa kuhakikisha elimu ya Bima ya Afya kwa wote inawafikia wananchi wote ili waweze kuuelewa na kuutumia ipasavyo.
Aidha, amewasisitiza wanufaika kutumia vitambulisho vya bima kwa uaminifu na kuvitunza vizuri, akionya kuwa vitambulisho hivyo vinapaswa kutumiwa na walengwa halali pekee.
“Huduma itatolewa kwa mmiliki wa kitambulisho pekee. Isitokee kumpa ndugu, rafiki au mtu mwingine asiyehusika kutumia. Endapo itabainika, hatua za kisheria zitachukuliwa,” amesema Gembe.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Dkt. Alex Alexander, amesema Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kugharamia walengwa 7,921 wilayani Same, hatua itakayowawezesha wananchi wasio na uwezo kupata huduma za afya bila kulipia.
Naye Diwani wa Kata ya Stesheni Mhe.Saida Magiri ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutekeleza mpango huo kwa vitendo, akisema mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unalenga kuboresha afya na ustawi wa wananchi wenye mahitaji maalum.
Serikali ilitangaza kuanza rasmi kwa utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa wote kuanzia Januari 26, 2026. Kupitia mpango huo, kaya zitajiunga kwa kulipa shilingi 150,000 kwa mwaka kwa kaya isiyozidi watu sita, huku wananchi wasio na uwezo wakigharamiwa na Serikali.
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.