Wilaya ya Same imejipanga kuongeza uzalishaji wa zao la Mkonge kutoka Tani 1,351 za sasa hadi kufiki tani 2,500 mwaka 2030 ili kupanua wigo wa upatikanaji wa mazao ya Viwanda na kuinua wananchi kiuchumi.
Zao la Mkonge ni zao la kimkakati kwenye Wilaya ya Same ambapo tayari Wilaya imetenga Ekari 4,000 kwenye Kata ya Makanya lenye vitalu 162 ambapo tayari vitalu 158 vimeshakodishwa kwa wawekezaji wa ndani ili kuongeza mapato ya Halmashauri.
Afisa Kilimo, Uvuvi na Mifugo wa Wilaya ya Same Dkt. Cainan Kiswaga amesema vitalu hivyo vimekondihwa kwa wadau 121 wa zao la Mkonge na vitalu vine vimetengwa kwaajili ya uzalishaji wa miche ya Mkonge ili kurahisisha upatikanaji wa miche.
Uanzishwaji wa zao la Mkonge kama zao la kimkakati unatokana na agizo la Waziri Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa ambapo alielekeza kila Wilaya hapa nchini kuwa na mazao ya kimkakati ili kukwamua wananchi kiuchumi.
“Tunaishukuru sana Bodi ya Mkonge hapa nchini kwa kutupatia miche 135,000 ya Mkonge ambayo imeweza kufikia wakulima 25 wa Mkonge kutoka Kata za Makanya,Saweni na Hedaru” alisema Dkt. Kiswaga.
Amesema kuwa katika kurahisisha uendeshaji na usimamizi wa uzalishaji wa zao la Mkonge Halmashauri imesimamia uanzishwaji wa ushirika wa Wakulima wa mkonge unaojulikana kama SAME SISAL AMCOS.
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.