Kufuatia mahitaji makubwa ya miche ya zao la Parachichi Halmashauri ya Wilaya ya Same imeandika maombi Wizara ya Kilimo kuomba kusaidiwa miche 56,289 ya Parachichi zinazokomaa muda mfupi ili kuweza kuisambaza kwa wananchi.
Tangu mwaka 2022 Wilaya ya Same imeliweka zao la Parachichi kmiongoni mwa mazao ya kimkakati ya kuinua uchumi wa Wananchi wa ukanda wa milimani kwenye Wilaya ya Same.
Baada ya zao hilo kutangazwa kama zao la kimmkakakti lenye lengo la kuinua uchumi wa Wakulima tayari jumla ya miche 5,822 imeshaoteshwa kenye maeneo mbalimbali ambapo miche hiyo ilitolewa na wafadhili mbalimbali wakiwemo Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki (EAMCEF) pamoja na Shirika la Forest Focus.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya WIlaya ya Same Bw.Jimson Mhagama amesema mwamko wa wananchi kuotesha Parachichi zinazokomaa muda mfupi ni mkubwa sana ndio maana tumeamua kuomba Msaada wa Wizara ili kupata miche zaidi.
“Tuna Kata zaidi ya 12 za ukanda wa milimani ambao una baridi ambapo utafiti umeonyesha kwamba hizi Parachichi zinaweza kustawi na tayari wananchi tumewahamasisha kupanda parachichi hizi na mwamko umekuwa mkubwa” alisema Mhagama.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Mheshimiwa Yusto Mapande ameahidi kufuatilia maombi hayo ya Miche Wizara ya Kilimo ili wananchi waweze kupatiwa.
Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Wilaya ya Same, Dkt.Cainan Kiswaga alisema miche ya Parachichi inayokomaa mapema ni chachu ya kuinua wananchi kiuchumi kwani mti mmoja wenye miaka mine unaweza kuzaa matunda 400 kwa mwaka na uzalishaji huongezeka kwa kadri umri wake unavyoongezeka ambapo mti wa miaka saba huzaa matunda hadi 800 kwa mwaka wakati miti ya asili ina uwezo wa kuzaa matunda 150 tu kwa mwaka.
Alizitaja Kata ambazo zao la Parachichi linastawi kuwa ni pamoja na Mshewa,Mhezi,Msindo,Vuje,Mtii,Bombo,Bwambo,Mpinji,Chome,Vudee, Vunta, Suji na Myamba.
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.