Katika jitihada za kuboresha kilimo na kuinua uchumi wa wakulima Halmashauri ya Wilaya ya Same imegawa Kanda tatu za Uchumi wa Kilimo ambazo wakulima wanapewa elimu juu ya aina ya mazao ya biashara yanayoweza kustawi katika Kanda hizo.
Akizungumza katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini yaliyofanyika katika viwanja vya Themi,Njiro mkoani Arusha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Mhe. Yusto Mapande alisema kwa muda mrefu wakulima wilayani humo wamekuwa wakilima kilimo cha mazoea ambacho hakijaweza kuwainua kiuchumi.
“Tumeamua kugawa Kanda tatu za kilimo ambazo ni Ukanda wa Tambarare ambao unalimwa Mkonge na mbogamboga katika eneo la umwagiliaji la Ruvu,Ukanda wa Kati ambao unalima Mpunga na Ukanda wa juu milimani ambao unalima Tangawizi na kwa sasa tunahimiza sana kilimo cha parachichi na tayari tumeshaanzisha vitalu vya miche ya parachichi” alisema Mapande
Amesema ili kufanikisha malengo ya kuinua uchumi wa wakulima Halmashauri inatengeneza miundombinu ya umwagiliaji ili kuwasaidia wakulima kuondokana na kilimo cha mazoea cha kutegemea mvua za msimu.
“Sambamba na kuboresha miundombinu pia tunahakikisha wakulima wanapata pembejeo za kilimo kwa wakati ambapo tunatumia mawakala wa pembejeo waliopo katika maeneo yetu yote” amesema Mhe.Mapande.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Bi.Anastazia Tutuba amesema maafisa Ugani wa Halmashauri waliopo katika Kata wamekuwa wakiendelea kutoa elimu kwa wakulima juu ya njia mbalimbali za kuboresha kilimo.
“Njia nyingine ya kutoa elimu kwa wakulima wetu ni kupitia maonesho haya ya Nanenane,hapa tumekuja na wakulima wetu ambapo pamoja na kutangaza bidhaa zao lakini wanajifunza mbinu mbalimbali za kilimo kutoka kwa wenzao wa maeneo mengine” amesema Bi.Tutuba.
Mkurugenzi huyo amesema kwa mwaka wa fedha ulioishia June 2023, Divisheni ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi ilitumia shilingi milioni 116 katika kuboresha kilimo na ufugaji wilayani humo.
Akizungumza katika Maonesho hayo, Mwenyekiti wa wakulima wa Tangawizi Kata ya Myamba Bw.Mbaraka Ally amesema "Faida kubwa ya kushiriki maonyesho ya nanenane ni kutangaza bidhaa yetu ya Tangawizi ambayo inatoka Mamba-Myamba, ambapo Tangawizi yetu ina ubora wa hali ya juu”
Bw.Eliniokoa Joseph ambaye ni Mkazi wa Arusha anasema" Nimekuja kwenye Banda la Maonesho la Same mahususi kwa ajili ya kununua Tangawizi ya Same, nimeshaitumia,ni nzuri sana na inaponya mafua na magonjwa madogo madogo ni nzuri".
Maonesho ya Nane nane ya mwaka 2023 yamebebwa na kaulimbiu isemayo “Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu wa Chakula”
The Way Through Mkomazi Nationa Park or District Hospital(Kibacha Rd)
Sanduku La Posta: P.O.Box 138
Simu ya mezani: +255 27 2758034
Simu Ya Mkononi: +255 717657681
Email: ded@samedc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.