Kaimu Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Edward Mpogolo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Same amekabidhiwa na kuzindua vyumba 56 vya madarasa katika shule 36 za sekondari halmashauri ya Same, huku akiwapongeza wasimamizi wa mradi huo kuanzia ngazi ya wilaya, halmashauri, kata, viongozi wawakilishi wa wananchi pamoja na wananchi wote kwa ushiriki wao, kwa kukamilisha miradi hiyo kwa viwango na kwa wakati.
Mkuu huyo wa mkoa, ametoa pongezi hizo mara baada ya kuridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa ya Mpango wa Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19, ambapo alipokea na kuzindua madarasa 56, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi hiyo katika halmashauri ya Same.
"Ninawapongeza wananchi wote wa halmashauri ya Same kwa ushirikiano mliouonesha katika kutekeleza mradi huu wa ujenzi wa madarasa, madarasa yamejengwa kwa viwango vinavyohitajika na kukamilika kwa wakati, madarasa yanavutia, hii inaonesha dhahiri namna gani mnaunga mkono agenda ya mheshimiwa Rais, mama Samia ya kuboresha huduma za jamii na kuondoa kero kwa wananchi, hongereni sana ofisi ya mkuu wa wilaya, timu ya watalamu halmashauri, waheshimiwa madiwani pamoja na wananchi wote kwa ujumla wenu" amesisitiza Mhe. Mpogolo.
Aidha, mheshimiwa Mpogolo amewataka wananchi kuendelea kushiriki utekelezaji wa miradi yote inayotekelezwa katika maeneo yao, kwa kuwa serikali imeleta fedha nyingi katika miradi ya elimu, afya, maji na barabara, serikali inahitaji ushiriki wa wananchi, ushiriki ambao utawezesha umiliki wa wananchi wa miradi hiyo baada ya kukamilika.
Katika ziara hiyo viongozi wawakilishi wa wananchi, wameipongeza na kuishukuru serikali ya awamu ya sita na juhudu za mhesimiwa Rais, mama Samia Suluhu kwa kuelekeza fedha nyingi, kiasi cha shilingi bilioni 1,120 milioni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za halamshauri ya Same, jambo ambalo wamekiri halijawahi kutokae na kuongeza kuwa, fedha hizo za ujenzi wa madarasa zimekuja wakati muafaka kwa kuwa kila mwaka, wananchi hulazimika kuchangishana kujenga madarasa ya kidato cha kwanza kwa mwaka unaofuata.
Diwani wa kata ya Msindo Mhe. Yusto Mapande ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri amesema kuwa licha ya kuwa madarasa hayo yatawanufaisha watoto wao, lakini kwa kiasi kikubwa yamewapunguzia wananchi mzigo wa kuchangishana fedha za ujenzi wa madarasa, zoezi ambalo hufanyika kila mwaka nyakati kama hizo.
Ikumbukwe kuwa, halmashauri ya Same ilipokea shilingi bilioni 1,120 milioni, fedha za Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19, za ujenzi wa vyumba 56 vya madarasa kwa shule za sekondari na madarasa yote yanatakiwa kukamilika ifikapo 31, Desemba, 2021.
SAME DC
Kazi Iendelee.
The Way Through Mkomazi Nationa Park or District Hospital(Kibacha Rd)
Sanduku La Posta: P.O.Box 138
Simu ya mezani: +255 27 2758034
Simu Ya Mkononi: +255 717657681
Email: ded@samedc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.