Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Kilimanjaro Bw. Kiseo Nzowa amepongeza utekelezaji wa Miradi Wilayani Same wakati alipofanya ziara ya siku moja ya kutembelea na kukagua Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa Wilayani Same.
Katika ziara hiyo RAS Nzowa alitembelea Ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Amali ya Kihurio ambayo Ujenzi wake unagharimu Mil. 584.28 fedha kutoka Mradi wa SEQUIP na ujenzi wake umefikia asilimia 95.
Miradi mingine iliyotembelewa ni Mradi wa Bwalo la Chakula kwenye Shule ya Sekondari Ndungu ambao unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi mil. 195 ambapo kati ya fedha hizo Mil. 170 zimetoka Serikali Kuu na Mil 25 zimetokana na mapato ya ndani ya Halmashauri.
Katibu Tawala Nzowa alihitimisha ziara yake kwa kutembelea Mradi wa Ujenzi wa Kidato cha tano na sita kwenye Shule ya Sekondari Misufini Goma ambao umegharimu Shilingi Milioni 389.4 kutoka SEQUIP.
Miradi yote iliyotembelewa ujenzi wake umekamilika kwa zaidi ya asilimia 95 ambapo Katibu Tawala aliipongeza Halmashauri kwa usimamizi mzuri wa Miradi na kuelekeza hatua ya umaliziaji kuhakikisha kuwa majengo yote yanawekwa sakafu ya marumaru(tiles).
"Naona Miradi hii ipo kwenye hatua za umaliziaji, hivyo hakikisheni inakamilika kwa wakati ili iweze kupokea wanafunzi mwakani" alisema Nzowa.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Same Mheshimiwa Kasilda Mgeni aliishukuru Serikali kwa kuipatia Wilaya ya Same Miradi itakayowezesha wanafunzi wengi zaidi kujiunga na Elimu ya Sekondari pamoja na kunufaika na Elimu ya Amali (Ufundi).
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.