Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Bi.Anastazia Tutuba ameyapongeza mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO's) zinazofanya kazi katika Wilaya ya Same kwa kushiriki katika kufanikisha shughuli mbalimbali za maendeleo Wilayani humo.
Akizungumza wakati akifungua Kikao cha viongozi wa NGOs Feb 20,2024 Mkurugenzi huyo alisema mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika maendeleo ni mkubwa.
"Serikali ina wajibu wa kuhakikisha inawaletea maendeleo wananchi wake,lakini tunashukuru sana NGO's zimekuwa na ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha wanaunga mkono jitihada za serikali"alisema.
Bi.Tutuba alisema kuwa bado Serikali inahitaji mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika kutokomeza umaskini, njaa na changamoto nyingine zinazoikabili jamii.
Akizungumza katika kikao hicho kilichojumuisha wawakilishi kutoka NGOs zaidi ya 30 Mratibu wa Jukwaa la Maendeleo Endelevu Tanzania (UNA-TANZANIA SUSTAINABLE PLATFORM)Bi.Judith Urio alisema kikao hicho kimelenga kujua NGOs zilizopo kwenye Wilaya ya Same na kujua shughuli zinazofanya na mashirika hayo.
Alisema lengo ni kurahisisha katika kuyaunganisha mashirika hayo na wafadhili au Serikali pale inapohitajika kufikisha huduma mbalimbali kwa Jamii.
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.