Wajumbe wa Baraza la Mji mdogo Wilaya ya Same wameomba Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) kuongeza bajeti ya utengenezaji wa barabara za mitaa na uwekaji Mitaro kwenye barabara hizo.
Wakizungumza kwenye kikao hicho wajumbe hao walisema zipo barabara kubwa za mitaa ambazo zikitengenezwa kwa kiwango cha lami zitapunguza msongamano kwenye barabara kuu.
Waliitaja barababara inayotokea mnada wa kwasakwasa kuelekea chuo cha FDC hadi kuungana na barabara ya Mwembe kuwa inatumiwa na watu wengi sana hivyo ikitengenezwa kwa kiwango cha lami itapunguza msongamano wa magari toka barabara kuu iendayo Dar es salaam.
Akizungumza kwenye Kikao hicho Mjumbe wa Mtaa wa Mbuyuni Kata ya Stesheni alisema kuna umuhimu mkubwa wa kutengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha lami na pia mitaro yake iboreshwe.
Akizungumza kwenye kikao hicho Meneja wa TARURA WIlaya ya Same Mhandisi James Mnene alisema bado mahitaji ya barabara za lami na ujenzi wa mitaro ni makubwa lakini TARURA inaendelea kujenga kwa kadri inavyopokea bajeti.
"Changamoto kubwa ni ufinyu wa bajeti lakini tunaendelea kuomba tuongezewe bajeti ili tuweze kuimarisha mitandao yetu ya barabara na mitaro ya maji ya mvua" alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo Mheshimiwa Ramadhani Mangare alitoa wito kwa TARURA kuhakikisha wanaboresha barabara za mitaa ziweze kupitika msimu wote wa mwaka.
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.