Ujio wa Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt.Philip Mpango kwenye Wilaya ya Same umeleta neema kwa Shule ya Sekondari Same kuchimbiwa visima vya maji baada ya shule hiyo kukosa maji ya uhakika kwa muda mrefu.
Dkt.Mpango alifika kwenye shule ya Sekondari Same kuotesha mti kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na siku ya upandaji miti kitaifa ambapo pia alipata ,muda wa kuongea na wanafunzi wa shule hiyo kongwe yenye wanafunzi wa kidato cha tano na sita wapatao 950 ambayo ilianzishwa mwaka 1952.
Wanafunzi hao walitumia fursa hiyo vizuri ambapo waliwasilisha kilio chao cha ukosefu wa maji ya uhakika jambo linalosababisha wakati mwingine wapeane zamu za kuoga.
Akitoa neno la shukrani kwa Makamu wa Rais kufika na kuotesha mti shuleni hapo, Mwanafunzi wa kidato cha sita Joshua Mwakijangala alimuomba Makamu wa Rais kusaidia upatikanaji wa maji shuleni hapo.
“Mheshimiwa Makamu wa Rais tumefurahi sana wewe kufika hapa shuleni kwetu,hapa shuleni tuna changamoto ya upatikanaji wa maji tunaomba utusaidie tupate maji ya uhakika” aliomba Mwanafunzi huyo.
Aidha mwanafunzi huyo aliomba pia Serikali kusaidia ukarabati wa mabweni au ujenzi wa mabweni mapya ili kuweza kukidhi uhitaji wa mabweni pia tunaomba kupatiwa walimu wa Sayansi.
“Tunashukuru Serikali imekarabati mabweni mawili makubwa na pia imetujengea bweni moja jipya lakini bado tuna uhitaji wa nyongeza ya mabweni” alisema Mwanafunzi Joshua.
Akijibu maombi hayo Makamu wa Rais Mheshimiwa Mpango alimwagiza Waziri wa maji Juma Aweso aliyekuwepo kwenye msafara huo kuhakikisha kuwa visima vinachimbwa shuleni hapo ambapo Waziri Aweso aliahidi utaratibu wa kuchimba kisima utaanza Machi 22,2024.
Kuhusu nyongeza ya mabweni Mheshimiwa Makamu wa Rais alisema serikali itaongeza mabweni ambapo pia aliagiza katika ajira mpya za walimu shule hiyo ipatiwe walimu wa Sayansi.
Siku ya Misitu Duniani na uoteshaji miti kitaifa huazimishwa Machi 21 ya kila mwaka na mwaka huu imeffanyika kitaifa wilayani Same,Kilimanjaro ikiwa na kaulimbiu isemayo “Misitu na Ubunifu”
The Way Through Mkomazi Nationa Park or District Hospital(Kibacha Rd)
Sanduku La Posta: P.O.Box 138
Simu ya mezani: +255 27 2758034
Simu Ya Mkononi: +255 717657681
Email: ded@samedc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.