Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini imeendesha mafunzo maalum kwa Viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Vitongoji, Wilayani Same, mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kudhibiti matumizi ya madawa ya kulevya.
Mafunzo hayo yamefanyika Mei 29, 2025, kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, yamelenga kuwawezesha viongozi hao kutambua, kuzuia na kushughulikia changamoto zinazotokana na matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Viongozi hao pia wamehimizwa kuzingatia maadili, uwajibikaji na ushirikiano wa kijamii katika mapambano hayo.
Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mheshimiwa Kasilda Mgeni, alisema kuwa dawa za kulevya si tu kwamba zina madhara ya kiafya kwa binadamu, bali pia zinachangia kudhoofisha uchumi, kuvuruga familia, kuporomosha maadili, kupunguza nguvu kazi ya Taifa na kuongeza matukio ya uhalifu.
“Hili ni janga linalohitaji nguvu ya pamoja kuanzia kwa viongozi, wazazi, walimu na vijana wenyewe ambao ndio waathirika wakuu wa dawa za kulevya.
Hivyo nawahimiza kupitia mafunzo haya mkawe mabalozi na waelimishaji; muhamasishe na msimamie utekelezaji wa mikakati ya kupambana na dawa za kulevya katika maeneo yenu.”
Aidha, aliwataka viongozi wa serikali kuhakikisha kuwa wanakuwa wawajibikaji, waadilifu na kutofumbia macho biashara haramu ya dawa za kulevya katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Afisa Elimu kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Kanda ya Kaskazini Bw. Shaban Miraji, alisema kuwa sababu kuu zinazochangia matumizi ya dawa za kulevya ni pamoja na malezi duni, ukosefu wa elimu sahihi kuhusu madhara ya dawa hizo, pamoja na hali ngumu ya kiuchumi.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015, mtu yeyote atakayekutwa akilima bangi au mirungi, kufanya biashara, kusafirisha au kumiliki kiasi cha bangi au mirungi kisichozidi kilo 100, atahukumiwa kifungo kisichopungua miaka 30. Iwapo kiasi hicho kitazidi kilo 100, adhabu ni kifungo cha maisha.@ortamisemi@maelezonews
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.