Mkuu wa Wilaya ya Same Mheshimiwa Kasilda Mgeni ameishukuru Wizara ya Afya na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kuratibu na kusimamia vema utoaji wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV)kwa mabinti ili kuwakinga na maambukizi ya virusi vinavyosababisha kansa hiyo.
Ametoa shukrani hizo wakati akizundua zoezi la chanjo ya saratani ya mlango wa uzazi kwenye wilaya ya Same ambapo alisema zoezi hilo limefanikishwa na Wizara ya Afya na TAMISEMI.
“Tunazishukuru sana Wizara hizi maana watumishi wake walio ngazi za wilaya na mikoa ndio wasimamizi na watekelezaji wakuu wa zoezi hili katika maeneo yao na wamekuwa wakifanya kazi zao kwa weledi mkubwa” alisema Mheshimiwa Kasilda.
Ametoa wito kwa wazazi na walimu kuhakikisha kuwa mabinti wote wenye umri wa miaka 9-14 wanapata chanjo hiyo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwani takwimu zinaonyesha kuwa kila mwaka wanawake Zaidi ya elfu kumi hugundulika kuwa na maambukizi ya saratani ya mlango wa kizazi.
Takwimu zinaonyesha kwa mwaka 2023 jumla ya wanawake 10,868 waligundulika kuambukizwa saratani ya mlango wa kizazi.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi inawalinda mabinti kutopata saratani hiyo ambayo inasababisha ugumba, upungufu wa damu na hata kupelekea kifo iwapo itampata mtu.
Awali akitoa taarifa fupi ya zoezi hilo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Same Dkt. Alex Alexander alisema zoezi hilo litafanyika kwa siku tano kuanzi April 22 -26 ambapo Wilaya inatarajia kuchanja mabinti 3,768.
“Tupo katika Maadhimisho ya wiki ya Chanjo Afrika ambayo hufanyika mwezi April kila mwaka na kwa mwaka huu sisis tumeamua kuchanja mabinti zetu ili kuwalinda na ugonjwa huu hatari” alisema Dkt.Alex
Akizungumza katika hafla hiyo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Dkt. Cainan Kiswaga alisema Wilaya imejipanga vema kuhakikisha kuwa mabinti wote wanaopaswa kuchanjwa wanapata chanjo ili kuwalinda na saratani hiyo.
Nae Afisa Afya wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Happinus Pilula amesema saratani ya mlango wa kizazi ndio saratani inayoongoza kwa kuua hapa nchini ambapo alisema kwa mwaka jana jumla ya wanawake 398 waligundulika kuwa na saratani ya mlango wa kizazi.
The Way Through Mkomazi Nationa Park or District Hospital(Kibacha Rd)
Sanduku La Posta: P.O.Box 138
Simu ya mezani: +255 27 2758034
Simu Ya Mkononi: +255 717657681
Email: ded@samedc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.