Mkuu wa Wilaya ya Same Mheshimiwa Kasilda Mgeni ameishukuru Kampuni ya Mtabe Group kwa kufadhili huduma ya uchunguzi kwa wananchi wa Kata ya Hedaru Wilayani Same na amewataka wananchi kutumia fursa hiyo vizuri ili waweze kujua hali zao kiafya.
Mheshimiwa Kasilda ametoa pongezi hizo wakati akizindua utoaji wa huduma hizo kwenye kituo cha Afya Hedaru ambapo alisema Kampuni hiyo imefanya jambo kubwa sana la kufadhili huduma hizo kwa wananchi wa Hedaru.
“Niwapongeze sana Mtabe Group kwa kujali afya za watanzania na kuamua kuja kufadhili huduma hii hapa Hedaru ili wananchi waweze kujua hali zao za afya” alisema Mhe.Kasilda
Aliwataka wananchi wa Hedaru kutumia vizuri fursa hiyo kwa kujitokeza na kupata huduma za uchunguzi bure na iwapo watagundulika na tatizo lolote waanze matibabu mapema.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo Katibu wa Chama Cha Madaktari Tanzania (MAT) Dkt. Nashivai Kivuyo alisema lengo la huduma hizo ni kusaidia kutambua mapema magonjwa yasiyoambukiza ili wananchi waweze kupata huduma mapema.
Alisema uchunguzi utakaofanyika ni wa magonjwa yasiyoambukiza lakini yamekuwa yakiathiri jamii kubwa ambayo ni Saratani, Shinikizo la damu na Kisukari .
“Tunatambua kuwa mtu ni afya na bila afya hakuna lolote litakaloweza kuendelea hivyo tumekuja kufanya uchunguzi wa magonjwa hayo kwani yanapogundulika mapema inakuwa ni rahisi kuyadhibiti”alisema Dkt. Kivuyo
Nae Mkurugenzi wa Mtabe Group Tanzania Bw.Gerald Aggrey alisema Kampuni yao imeamua kufadhili huduma ya uchunguzi kwa wananchi wa Hedaru ili waweze kujua hali zao kiafya na pia wapate elimu ya kutunza afya zao dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Akitoa taarifa za hali ya magonjwa yasiyoambukiza, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Same, Dkt Alex Alexander amesema kwamba kwa mwaka huu 2024 hadi kufikia tarehe 30 Octoba, kati ya Wagonjwa wa Nje (OPD) 200,391 waliohudumiwa katika Vituo mbalimbali vya kutolea huduma za Afya ndani ya Wilaya ya Same, Wateja 10,089 sawa na 5.03% walikuwa na Shinikizo la juu la damu (Hypertension), Wateja 3,885 sawa na 1.9% walikuwa na Ugonjwa wa Kisukari (Diabetes Mellitus) na Wateja 124 sawa na 0.01% walikua na Saratani za aina mbalimbali (Cancer).
Hivyo amewaasa wananchi wote wa Hedaru na Wilaya ya Same kwa ujumla kuzingatia namna bora ya maisha kwani magonjwa mengi yasiyoambukiza yanazuilika kwa kuwa na mtindo bora wa maisha kama kufanya mazoezi, kuzingatia lishe bora na kuepuka msongo wa mawazo.
Baada ya zoezi la uzinduzi wa huduma hizo kufanyika wananchi zaidi ya 50 walikuwa wamejiorodhesha kufanyiwa uchunguzi wa afya zao.
The Way Through Mkomazi Nationa Park or District Hospital(Kibacha Rd)
Sanduku La Posta: P.O.Box 138
Simu ya mezani: +255 27 2758034
Simu Ya Mkononi: +255 717657681
Email: ded@samedc.go.tz
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.