Baraza la Madiwani lililomaliza muda wake Wilayani Same limeidhinisha kupandishwa Madaraja kwa watumishi zaidi ya 1,000 wa kada mbalimbali ndani ya Halmashauri ili kuongeza morali na ufanisi kazini.
Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kabla ya kuvunjwa kwake Juni 20,2025 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Mheshimiwa Yusto Mapande, amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha haki na stahiki za watumishi zinalindwa kwa kuzingatia uwajibikaji na utendaji wa mtu mmoja mmoja.
“Tumekuwa tukipima utendaji wa kila mtumishi kwa kuzingatia vigezo halali, watumishi waliopandishwa madaraja wamekidhi vigezo, na tutaendelea kuhakikisha tunatoa motisha kwa wanaojituma kwa bidii kazini,” alisema Mhe.Mapande.
Ameongeza kuwa Halmashauri itaendelea kufanya tathmini ya mara kwa mara kwa watumishi wake ili kuhakikisha ufanisi unabaki kuwa kigezo kikuu cha maendeleo ya taasisi hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa maadili na nidhamu kazini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bw.Jimson Mhagama alisema upandishwaji Madaraja Watumishi ni suala endelevu ambalo hufanyika kila mwaka ili kuongeza morali ya kazi.
"Kuwapandisha Watumishi madaraja ni takwa la kisheria lakini pia inawaongezea Watumishi morali ya kufanya kazi"alisema Mhagama.
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.