Wananchi Wilayani Same wameonywa kutotumia njia zisizo rasmi kuunganishiwa huduma ya Maji kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na watakaobainika hatua Kali zitachukuliwa dhidi yao.
Onyo hilo limetolewa Juni 16, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Same, Mheshimiwa Kasilda Mgeni, wakati wa kikao cha wadau wa maji kilichoandaliwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (SAMWASA) wilayani humo.
Mhe. Kasilda amesema vitendo vya wizi wa maji vimekuwa kikwazo kikubwa kwa Mamlaka hiyo kufikia malengo ya utoaji wa huduma bora ya maji kwa wananchi.
"Kuharibu miundombinu ya maji au kujiunganishia maji kwa njia ya wizi ni kosa kisheria na ukikutwa utashtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi"alisema Mhe. Kasilda
Aidha, amewataka wananchi kulipa ankara za maji kwa wakati ili kuwezesha mradi wa maji wa Same -Mwanha-Korogwe (SMK) kujiendesha kwa ufanisi na kuongeza mtandao wa huduma kwa maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma hiyo muhimu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa SAMWASA, Mhandisi Rashid Mwinjuma amesema kuwa changamoto ya wizi wa maji inaisababishia mamlaka hiyo hasara kubwa kwa kuikosesha mapato, jambo linalokwamisha juhudi za upanuzi wa huduma kwa wananchi.
Ameeleza kuwaTaasisi hiyo itawachukulia hatua kali za kisheria watumishi wasio waadilifu wanaochangia hasara na kuharibu miundombinu ya maji, huku akitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za siri pindi wanapobaini vitendo vya ubadhirifu au hujuma dhidi ya miundombinu ya maji.
Sheria ya kuunganisha maji bila kibali ni kosa la jinai linaloweza kusababisha mtu kushtakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Uhujumu Uchumi na pia Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Na. 5 ya mwaka 2019.
Kwa mujibu wa sheria hizo, mtu yeyote anayejiunganishia maji kinyume cha taratibu, kuharibu miundombinu au kusababisha hasara kwa mamlaka ya maji, anatenda kosa linaloweza kumfikisha mahakamani na kuhukumiwa kwa kosa la jinai, ikiwa ni pamoja na kulipa faini au kifungo jela.
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.