Wadau wa madini Wilayani Same wametakiwa kuhakikisha kuwa wanatunza Mazingira kwenye maeneo wanayochimba madini kwa kufukia mashimo baada ya kumaliza kuchimba.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Same Mhe.Kasilda Mgeni kwenye kikao cha Wadau wa Madini ya Jasi (Gypsum),Pozolana na Bauxite ambayo hupatikana kwa wingi Wilayani Same ambao wamekutana kujadili changamoto mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi.
Amesema utunzaji wa Mazingira ikiwemo ufukiaji wa mashimo baada ya kuchimba madini ni muhimu kwani itasaidia utunzaji wa maeneo hayo.
"Pamoja na utunzaji wa Mazingira hakikisheni pia mnalipa kwa wakati maduhuli yote ya Serikali ili kukuza uchumi wa nchi"alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Akizungumza kwenye kikao hicho Afisa Mkazi wa Madini Mkoa wa Kilimanjaro (RMO) Mhandisi Abel Madaha amesema uchimbaji Madini umekua ukichangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa ambapo kwa mwaka 2024/2025 hadi kufikia mwezi April 2025 sekta ya Madini Mkoani humo imekusanya Tsh.Bil.3.2 ambayo ni asilimia 91 ya lengo la kukusanya Tsh.Bil.3.5
Alisema asilimia 31 ya mapato hayo inatokana na mapato ya Madini ya Jasi.
Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Makanya ambayo inazalisha kwa wingi Madini ya Jasi Mhe. Damar Kingalu amewaomba wazalishaji wa Jasi kurejesha kiasi cha faida kwa Jamii (CSR) ili kuboresha maisha ya wananchi katika eneo hilo.
Kikao hicho kilichowakutanisha Wadau wa madini ya Jasi zaidi ya 50 wakiwemo wawakilishi wa Viwanda vya Saruji (Moshi,Twiga na Tanga Cement) kimeandaliwa na Tume ya Madini kwa kushirikiana na Chama cha Ushirika wa wachimbaji wa Jasi Mkoa wa Kilimanjaro (Kilimanjaro Gypsum Cooperation Society).
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.