Afisa Lishe Wilaya ya Same Bi.Jackline Kilenga amesema idadi ya wanafunzi wanaopatiwa chakula cha mchana shuleni imeongezeka na kufikia asilimia 98.
Aliyasema hayo katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa afua za lishe ambapo alisema afua nyingine zote zilikuwa zikifikia utekelezaji wa asilimia 100 lakini suala la wazazi kuchangia chakula shuleni lilikuwa ni changamoto lakini kwasasa hali ni nzuri.
Amesema kwa upande wa utoaji wa matone ya nyongeza ya vitamin A na utoaji wa dawa za minyoo kwa watoto umefanyika kwa asilimia 128.
Amesema kwa upande wa wajawazito imefanikiwa kuwapatia madini ya chuma na asidi ya foliki kwa asilimia 100.
Bi. Kilenga ametaja shughuli nyingine zilizotelezwa kuwa ni ukaguzi wa maeneo ya vyakula na Elimu ya ulishaji sahihi wa watoto wa changa na wadogo.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo Mkuu wa Wilaya ya Same Mheshimiwa Kasilda Mgeni aliwaagiza Watendaji wa Kata kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanapata chakula cha mchana shuleni ili Wilaya ifikie asilimia 100.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Bw.Jimson Mhagama aliwataka wazazi kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha kuwa wanachangia chakula ili kuwawezesha watoto wao kupata mlo wa mchana shuleni.
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.