Kaimu Afisa Tawala wa Wilaya ya Same Bw.Sixbert Sarmett amewataka Wakala wa Misitu (TFS) Kanda ya Kaskazini kuhakikisha kuwa wanasambaza miche ya miti kwenye Taasisi zote za Serikali na binafsi Wilayani humo ili kuendelea kutunza mazingira.
Alitoa wito huo kwenye zoezi la upandaji miti kwenye shule ya msing Kisima ikiwa ni mwendelezo wa kampeni maalum ya uoteshaji miti ili kuifanya Wilaya ya Same kuwa ya kijani ambapo alisema mvua za vuli zilizoanza kunyesha ni lazima zitumike vizuri kutunza mazingira.
Akimwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo Mheshimiwa Kasilda Mgeni kwenye zoezi hilo Bw.Sarmett kwa kushirikiana na TFS na wadau wa mazingira pamoja na wanafunzi walifanikiwa kuotesha miti 250.
“ Lengo la Wilaya ni kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka ambapo mwaka jana tulifanikiwa kupanda miti milioni 1.4 na mwaka huu tunatarajia tufikie lengo letu la kuotesha miti milioni 1.5” alisema na kuwapongeza TFS kwa kuwezesha upatikanaji wa miche ya kutosha.
Aidha Bw.Sarmett alizitaka mamlaka kuhakikisha kuwa hatua kazi zinachukuliwa kwa wale wote wanaoharibu mazingira kwa kukata miti hovyo na wanaochoma mkaa.
Akizungumza kwenye zoezi hilo Meneja wa TFS Kanda ya Kaskazini Bw. James Nshare alisema taasisi hiyo itaendelea kusambaza miche ya miti kwenye taasisi zote kama ilivyoelekezwa.
“Na watu binafsi pia wanaohitaji miche ya miti tunawakaribisha waje tutawapatia bure”Alisema Bw.Nshare
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.