Wasafiri ambao wanatumia Barabara kuu ya Same- Dar Es Salaam wameonywa kuacha kutupa takataka wanapopita kwenye eneo hilo ili kuepuka Uchafuzi wa Mazingira pembezoni mwaka Barabara.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Usafi Duniani ambayo Wilayani Same yamefanyika kwenye Kata ya Hedaru,Afisa Afya wa Wilaya ya Same Bi.Yuster Malisa amesema magari yanayotumia barabara hiyo yamekuwa yakichafua Mazingira.
"Tayari tumeshaanza kuchukua hatua za kudhibiti utupaji wa taka toka kwenye magari na kuna abiria tayari tumewapiga faini na zoezi hili litaendelea hadi hii tabia itakapokoma"alisema Bi. Malisa.
Akizungumzia kadhia hiyo Mkazi wa Hedaru Bw.Clement Elisafi alisema wasafiri wamekua wakitupa sana taka kwenye maeneo yao.
"Naomba tuwekewe mabango mwanzo wa Wilaya na mwisho wa Wilaya kuonya hii tabia"alisema Bw.Elisafi.
Aidha Afisa afya huyo amewataka wananchi wote wa Wilaya ya Same kuhakikisha kuwa wanachangia ada ya ulipaji taka ili kuwezesha zoezi la uzoaji taka.
Amewaagiza maafisa Afya wa Kata kuhakikisha kwamba wanasimamia maeneo yao vizuri ikiwa ni pamoja kuchukua hatua za kisheria kwa wananchi wote wanaokiuka taratibu za afya.
Siku ya Usafi Duniani huadhimishwa Septemba 20 ya kila mwaka na mwaka huu inaadhimishwa kwa kaulimbiu isemayo "Uhai hauna mbadala,zingatia Usafi wa Mazingira, Mtu ni Afya"
Hakimiliki©2018 Halmashauri ya Wilaya ya Same.Haki zote zimehifadhiwa.